Swahili With Mariana: Mwandishi Mlezi wa Kiswahili
Na Felix Odhiambo
Mariana Kweyu ni mwalimu wa Kiswahili na anapenda watoto wadogo. Yeye ni mtu anayezungumza lugha zaidi ya moja na anapenda kushirikiana na wazungumzaji wa lugha zingine. Mariana anathamini ufundi na ubunifu wa waandishi hivyo, yeye ni mmoja wa wasomaji wa vitabu katika kikundi cha Nairobi Book Club. Yeye ni mwandishi chipukizi anayemiliki blogu ya WordPress iitwaye marianakweyu.wordpress.com. Yeye huandika hadithi fupi na ana idhaa ya YouTube iitwayo ‘Swahili with Mariana‘. Kila siku jioni, yeye hujitahidi kupakia video za dakika kutoka tatu mpaka kumi za masomo ya Kiswahili. Mpaka sasa yeye ameweza kupakia video zaidi ya arobaini zinazowasaidia wanajamii wanaoanza kujifunza Kiswahili kama geni. Video hizi ni rahisi kuelewa na zaidi, zimeambatanishwa na mazoezi na picha zenye mnato wa kuvutia.
Mbali na kazi za ufundishaji na utayarishaji wa kanda fupi za video, Mariana anapenda kusafiri akitalii, kuchunguza na kufurahia utamaduni wa watu na jamii mbalimbali. Safari yake ya uandishi ilianza rasmi Machi, mwaka wa elfu mbili na ishirini; wakati wa mkurupuko mbaya wa ugonjwa hatari wa korona. Wakati huo, alipata muda wa kukaa peke yake na kutafakari hali za maisha. Upweke huo ndio uliomzalia wazo la kuandika falau kitabu kimoja ama vingi – ili azidi kufundisha Kiswahili chake. Kadri muda ulivyozidi kusonga ndivyo Mariana alipozidi kuingiwa uchu wa kuandika mswada. Mariana alijiunga na matibaa ya Writers Guild Kenya.
Matibaa hayo yanayojishughulisha na kutoa mafunzo kwa waandishi wanaochipukia na kuwachapisha baadaye yalimpokea kwa viganja viwili na moyo wa maridhio. Baadaye alipomaliza mafunzo hayo Mariana alikuwa na uwezo mkubwa wa kuandika chochote kwa mtindo wowote; bora tu ana kalamu! Ingawa tajriba yake ilikuwa imekwea na kufikia hadhi ya kutaka kutambulika, Mariana aligotana ‘kipaji-kwa-kipaji’ na changamoto si haba. Changamoto iliyoongoza changamoto zote wakati ule ilikuwa kwamba ndio, ana uwezo wa kuhariri, lakini ahariri nini? Karatasi zitahaririwaje zikiwa tupu…?
Yeye aliamua kuanza kuandika kwanza. Aliandika kuhusu ndoto zake. Kila alipolala usiku aliota, asubuhi alizamia kuvuta kumbukizi za njozi zake, akazinakili na kuhifadhi kwenye nyaraka za Microsoft. Ingawa Mariana hakuona ndoto kila siku, alijaribu sana kuzidi na mtindo huo. Kule kunakilinakili ndoto zake ndiko kulikokoleza moto wa kuwahi kuwa mwandishi bora kama Said A. Mohammed.
Septemba ya mwaka wa elfu mbili na ishirini shule zilifunguliwa kwa zamu na masomo yakarejelewa; ingawa hayakurejelewa kikamilifu. Wakati huo akili za Mariana zilianza kumshawishi asome zaidi kazi za watangulizi wake katika tasnia ya uandishi. Hakupoteza muda, alianza kununua vitabu na kuvisoma. Mariana anaweza akashuhudia kwamba hakika safari ya uandishi inahitaji ujipangaji bomba zaidi ya mwanajeshi wa kuingia vitani. Kusomasoma, kunukuunukuu na kukariri maandishi ya magwiji waliomtangulia kuandika ndiko kumekuwa kuishi kwake.
Kwa sasa Mariana anaandika kazi nyingi za fasihi. Uandishi wa Mariana katika lugha ya kiswahili unalenga hasa, vijana wanaofuzu katika vyuo vikuu na kujumuika na jamii. Katika kazi zake za awali yeye amejaribu kudokeza futuko zinazokumba vijana wanapojaribu kutafuta maisha baada ya kukamilisha masomo ya ngazi za juu. Mariana anakiri paruwanja kwamba “kweli mtu hawi mtu bila watu”. Safarini amekutana na kutangamana na waandishi chipukizi, wakinzani na wachochezi wa vipaji ambao wamemtia shauku ya kuandikia dunia nzima! Aggrey Barasa ni miongoni mwa waandishi wanaochipukia kasi ambao wamesimama tisti katika hali zote na Mariana ili kuhakikisha uandishi wa kizazi kipya katika hali bora! Hata hivyo Barasa na Mariana wamelelewa na matibaa ya Writers Guild Kenya.
Kwa kuzingatia hali kwamba Mariana ni miongoni mwa vijana wenyewe, yeye anaandika masuala yanayowakumba vijana vihalisi kabisa! Mariana anaamini sana kwamba kwa kuandika na kuanika masaibu yanayokumba vijana, suluhu inaweza ikapatikana. Kwa sasa anatarajia kuchapisha mwongozo wa kujifunza lugha hivi karibuni. Mariana Kweyu ama kweli amevunja nazi, kwani anavyobugia tui ya wafwasi wengi katika mtandao wa YouTube kunampa sababu nyingi za kuishi na kuishi tena!
https://marianakweyu.wordpress.com/2020/10/02/basi-limemkana-dereva/
https://www.instagram.com/swahiliwithmariana/