Vijana, Kuungana na Maarifa ni Asili ya Mageuzi

Vijana, Kuungana na Maarifa ni Asili ya Mageuzi

Na Sitati Wasilwa

Wiki chache zilizopita, mwanahabari tajika, Linus Kaikai, alizungumzia swala la vijana katika uongozi, hususan katika siasa za Kenya. Katika maelezo yake, alikariri jinsi wanasiasa hawa vijana walivyofeli kutoa mwongozo mwafaka kwa nchi ambayo takribani asilimia sabini na tano ya idadi ya watu wana umri chini ya miaka thelathini na tano.

Bwana Kaikai aliwataja wanasiasa waliotwaa uongozi wa taifa na kuelekeza mageuzi wangali vijana wakiwemo Tom Mboya, Mwai Kibaki, James Orengo, Koigi Wamwere, Mwachengu Mwachofi, Chibule wa Tsuma, Wasike Ndombi, Lawrence Sifuna, Paul Muite, Anyang’ Nyong’o, Mukhisa Kituyi, Martha Karua, Farah Maalim na wengineo.

Kwa kuwasuta wanasiasa vijana, mwanahabari huyo anadai kwamba hawana itikadi yoyote inayoelekeza fikra zao ikilinganishwa na kizazi cha wanasiasa vijana waliopigania uhuru na mchakato wa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.

Naunga mkono kauli ya Bwana Kaikai. Ni nadra sana kuwapata wanasiasa vijana ambao wana msimamo dhabiti lakini inafaa tutilie maanani maswala tofauti tofauti, kwa mfano, umiliki na uongozi wa vyama vya kisiasa nchini ambao una msingi katika hali ya kutokuwa na usawa kijamii na kiuchumi.

Ikumbukwe kwamba hulka ya wanasiasa hawa vijana ni kioo cha hali halisia ya vijana wengi tu nchini. Licha ya kunung’unika na kuwashtumu wanasiasa vijana, kwa ujumla, vijana wengi nchini wanaenzi ukabila, ubadhirifu wa mali na fikra duni ambazo haziwezi kufanikisha mageuzi ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Ni nafasi tu za kisiasa ambazo wamezikosa!

Uchaguzi mkuu uliopita uliashiria kwamba Kenya bado ina mwendo mrefu kuwapata viongozi wa kisiasa ambao wana uwezo wa kutekeleza mageuzi. Naandika haya kwa kuzingatia kwamba wapiga kura wengi walikuwa vijana lakini hawakumanika kuwachagua viongozi bali ‘vikaragosi’ tu. Hii haimaanishi kwamba wanasiasa watendakazi hawakuchaguliwa. Wapo ingawaje wachache mno.

Niliaibika mara si moja kuwaona na kuwasikiliza vijana waliohitimu katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu wakieneza ujumbe ulioashiria upungufu fulani wa kimawazo. Ni dhahiri kwamba vyeti vya masomo na fikra halisi au imani katika itikadi endelevu zina utofauti mkubwa kama ardhi na mbingu.

Changamoto iliyopo katika jamii yetu ni wingi wa viongozi, vijana na wananchi kwa ujumla wasiopenda kusomasoma au kujikuza kimaarifa. Nathamini sana kusomasoma kwa sababu ni njia kuu ya kuongeza maarifa na kuwa mbunifu kimawazo.

Vijana sharti wajikwamue kutoka kwa utumwa wa kiakili kama wanapania kutekeleza mageuzi katika nyanja tofauti maishani. Kunao waliotajika katika taaluma ainati na kutoa uongozi mwafaka. Vilevile, baadhi ya vijana wanaenzi usomaji wa vitabu na bila shaka wana upeo wa aina yake kwa maswala ya sera za kijamii na kiuchumi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa na taasisi ya Kenya National Bureau of Statistics (KNBS), idadi ya Wakenya walio na umri chini ya miaka thelathini na tano ni takribani milioni 35.7. Kwa kuzingatia takwimu hizi, vijana wanaweza kuungana na kusahihisha uongozi wa nchi.

Wingi wa idadi ya vijana nchini hauwezi kuleta mageuzi ila kwa kujijenga kimaarifa. Maarifa haya yatajenga msingi imara wa ukichaa fulani unaohitajika kuleta mabadiliko ya tija.

Je, mabadiliko ya tija yanawezekana nchini? Ndoto hii itatimia tu vijana wakiungana na kujiimarisha kiitikadi. Vijana wanapaswa kutumia mitandao ya kijamii kujinufaisha kimawazo ila wasitumie majukwaa haya ya kidijitali kueneza upuzi na uyakinifu. Pili na muhimu, vijana wavipende vitabu. Masomo ya shuleni ni finyu sana kuwezesha kufikiri kwa kina na wanaweza kuvianzisha vilabu vya usomi au hata kuvinunua vitabu. Haina maana kununua mavazi ya senti yatakayochakaa baada ya muda mfupi bila kuzingatia angalau kununua nakala ya kitabu!

 

Mwandishi ni mchumi wa kisiasa na mshauri wa maswala ya utawala, kanda-siasa na sera za umma. Vilevile, ni kiongozi wa vijana katika shirika la YMCA Kenya. Mitandao ya kijamii; Twitter: @SitatiWasilwa; Facebook: Sitati Wasilwa; LinkedIn: Sitati Wasilwa.

Suggested reads:

2 thoughts on “Vijana, Kuungana na Maarifa ni Asili ya Mageuzi”

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Open chat
1
Need help?
Writers Guild Kenya
Hello.
How can we help you?